Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah al-Udhma Hajj Sheikh Ja’far Subhani, miongoni mwa Mara’ji’ wakuu wa Kishia, katika ujumbe alioutoa jioni ya Jumatano, tarehe 4 Azar, kwa Mkutano wa Kitaifa wa “Falsafa ya Theolojia ya Kijamii kwa Msisitizo wa Mawazo ya Kitheolojia ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu”, uliofanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Utamaduni na Fikra za Kiislamu, amesema:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
يَرْفَعِ اللهُ الَّذِینَ آمَنُوا مِنکُمْ، وَالَّذِینَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجاتٍ
“Mwenyezi Mungu atawapandisha daraja wale walioamini miongoni mwenu, na wale waliopewa elimu.”
Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye alikamilisha dini Yake kwa kutumwa Mtume wa mwisho wa Manabii (s.a.w.w.), na akaitimiza neema Yake kwa wanadamu wote. Rehema na amani zimshukie Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.), ambao ni warithi wa kweli wa maarifa ya Mwenyezi Mungu na wabeba bendera ya Tawhidi na uadilifu katika zama zote.
Jukumu kuu la elimu ya Theolojia ya Kiislamu ni kufafanua na kutetea kwa hoja za kiakili misingi na maarifa ya kiitikadi, pamoja na kujibu shubha na pingamizi zinazolenga misingi ya dini. Elimu ya Theolojia ya Kiislamu ni elimu yenye heshima kubwa, ambayo humpa mwanazuoni wa dini uwezo wa kutetea eneo takatifu la itikadi kwa kutumia hoja na ushahidi wa kimantiki.
Elimu hii ilianza kujengeka na kukua tangu mwanzoni mwa Uislamu, kwa kutegemea Qur’ani Tukufu, Sunna za Mtume na mwenendo wa Ahlul-Bayt (a.s.). Qur’ani Tukufu, kupitia mijadala na hoja zake zinazothibitisha Umoja wa Mwenyezi Mungu, iliweka misingi ya fikra za Kitheolojia. Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), kupitia mijadala yake na washirikina pamoja na Watu wa Kitabu, na kwa kujibu mahitaji ya Waislamu, hata kama yalikuwa machache na ya awali, alifungua njia ya kutetea itikadi kwa njia ya kielimu. Nao Maimamu Maasumu (a.s.), kupitia barua na maelezo yao, waliimarisha misingi ya dini.
Kwa hiyo, Theolojia ya Kiislamu ni urithi halisi na wa kudumu ambao daima umekuwa katika mstari wa mbele katika kufafanua na kuitetea dini. Haja ya jamii ya Kiislamu kwa elimu hii haijawahi kupungua hata siku moja.
Bila shaka, elimu ya Theolojia, kama zilivyo elimu nyingine, haikusimama katika kipindi chote cha historia. Badala yake, imeendelea kupanuka kutokana na kukutana na dini mbalimbali, falsafa, tamaduni na maswali mapya yaliyojitokeza.
Hapa ni lazima tutofautishe mambo mawili: Kwa upande mmoja, kukubali umuhimu wa kujadili masuala mapya ya Theolojia ni jambo lisiloepukika. Hii ni kwa sababu shubha za kidini katika kila zama hujitokeza katika sura mpya; elimu za majaribio huibua maswali kuhusu Mwenyezi Mungu, uumbaji na mwanadamu; mikondo mipya ya kifalsafa huipinga misingi ya kimapokeo ya maarifa ya kidini; na mabadiliko ya kijamii na kiutamaduni huibua masuala mapya kuhusu dini na maisha.
Mwanatheolojia wa zama hizi, pamoja na kuufahamu urithi wa Theolojia wa zama zilizopita, anapaswa pia kuyafahamu mawazo mapya na kuyajibu kwa kutumia silaha ya akili na hoja za kimantiki.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, kupanuka kwa masuala haya hakumaanishi kwamba kumezaliwa elimu mpya ya “Theolojia ya Kiislamu” iliyo huru kabisa na tofauti na ile ya awali. Hii ni kwa sababu mada na jukumu la msingi la elimu ya Theolojia bado vinaendelea kuhifadhiwa. Kinachobadilika ni masuala na maswali mapya yanayoongezwa katika elimu hii katika kila zama.
Elimu ya Theolojia ni elimu hai, inayoendelea na yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na masuala mapya katika kila kipindi, na kutetea uwezo wa dini katika kuyajibu. Jambo muhimu ni kwamba mafundisho ya Kitheolojia yanapaswa kuwa msingi wa utekelezaji wa mambo na kufanya maamuzi. Dini ya Uislamu ni dini iliyokamilika na inayojumuisha nyanja zote za maisha; inahusu maisha ya mtu binafsi na yale ya kijamii. Kuifungia dini katika eneo la maisha binafsi na masuala ya mtu mmoja mmoja hakupatani na misingi ya Kitheolojia ya Uislamu.
Imani ya kidini ina nafasi muhimu katika kuwajibika kijamii, kupanga mahusiano baina ya wanadamu, kupambana na ufisadi, na kuimarisha utaratibu pamoja na mshikamano wa kijamii. Haya yote ni miongoni mwa majukumu ya kijamii ya mafundisho ya kiitikadi.
Kwa mtazamo huu, Theolojia ya Kijamii haipaswi kuchukuliwa kuwa ni elimu huru inayosimama sambamba na elimu ya jadi ya Theolojia. Badala yake, inapaswa kuchukuliwa kuwa ni mwendelezo wa kupanuka kwa wigo wa masuala yanayojadiliwa katika elimu ya Theolojia.
Kama ambavyo katika kipindi chote cha historia masuala mapya ya Kitheolojia yameongezwa katika elimu hii bila kubadilisha utambulisho wake, vivyo hivyo masuala ya kijamii yanaweza kuwa mada za uchunguzi wa Kitheolojia, na mafundisho ya kiitikadi ya Uislamu yana uwezo wa kuyajibu.
Kuingia katika masuala ya jamii hakumaanishi kubadilika kwa asili na utambulisho wa elimu ya Theolojia. Badala yake, mwanatheolojia anapaswa kuyachambua masuala mapya ya kijamii kwa kutumia misingi ya kiitikadi ya Uislamu.
Hata hivyo, ili uwezo huu uweze kugeuzwa kuwa mfumo madhubuti na wenye mshikamano wa Theolojia ya Kijamii, ni lazima kuandaliwa mijadala maalumu kuhusu mada zake, mbinu zake na malengo yake. Jambo hili linahitaji tafiti nzito na zilizopangwa kwa utaratibu maalumu. Tunatumaini kwamba mikutano kama huu unaofanyika sasa itakuwa msingi wa kufanikisha lengo hilo.
Ni dhahiri kwamba jukumu hili zito haliwezi kutekelezwa bila kuwaandaa wataalamu wenye ujuzi maalumu na bila kutumia uwezo wote wa kielimu uliopo katika Hawza na vyuo vikuu.
Kama ambavyo Imam Swadiq (a.s.) katika kipindi kigumu alichopitia aliwaandaa wanafunzi kama Hisham bin Hakam ili kutetea misingi ya itikadi kwa njia ya kielimu, vivyo hivyo leo hii Hawza za kielimu zinapaswa kuingia katika uwanja huu zikiwa na wataalamu wa fani mbalimbali za kielimu, na kujibu shubha mpya kwa kutumia maarifa maalumu na hoja madhubuti.
Katika Theolojia ya Kijamii, kwanza kabisa tunapaswa kunufaika na Qur’ani, Sunna, Nahjul-Balagha na urithi wa Ahlul-Bayt (a.s.). Sambamba na hilo, tunapaswa kujitahidi kupata ufahamu wa kina kuhusu falsafa, mantiki, elimu ya maarifa, elimu ya mwanadamu, jamii na masuala ya kijamii.
Mimi binafsi, huku nikitoa shukrani zangu kwa waandaaji na washiriki wote wa mkutano huu wenye thamani kubwa, ninatumaini kwamba matunda ya kielimu ya mkutano huu itakuwa hatua yenye mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza Theolojia ya Kijamii, kufafanua uwezo wa dini katika nyanja za kijamii, na kujibu mahitaji ya fikra na itikadi ya jamii ya Kiislamu.
Wassalaam alaykum warahmatullahi wabarakaatuh.
Maoni yako